NENO LA LEO: KUSULUBISHA MASIKIO
Mithali 17:4 "Mtenda mabaya husikiliza midomo ya uovu;Na mwongo hutega sikio lake kusikiliza ulimi wa madhara."
Kama tulivyoona jana juu ya kusulibisha macho, leo tunaangalia kiungo kingine MASIKIO, kwa kusikia mtu anajengwa tabia au anaharibu tabia. Siku moja nilishuhudia mtoto mchanga, akitikisa kichwa na miguu baada kufunguliwa music kwa sauti ya juu, kumbe kila siku dada wa kazi anashindia kusikikiza music akiwa naye.
Ubongo wa mtoto huyo umejazwa Bongo flavour na ndiyo itakuwa mazoea na hatimaye tabia yake. Masikio ni njia pana inayolisha ubongo na kuukuza kitabia, ukizoea kusikiliza matusi, utakuwa na tabia ya kutukana, ukizoea kisikiliza music wa SENGELI, kila wakati utajikuta unaimba na kutembea kisengeli.
Pia kuna watu ambao masikio yao yamenyanyuka juu kama ya sungura, muda wote yametega kusikiliza na kunasa vimaneno kama antena, na kusambaza, watu wakiongea au mtu akiongea na simu, anatega sikio, akinasa tu hatulii anaenda kusambaza na kuvumisha maneno, hao ndio huitwa wambea, kila mara kusutwa.
Shetani anatumia masikio kuharibu tabia za wengi, utamsikia mtu anasema, nimesikia ila sina uhakika; huo ni uovu, kwa nini usikilize na usambaze maneno yasiyokuhusu na huna uhakika nayo?. Bila kuyasalimisha masikio kwa Kristo, maovu mengi yatakuwa ni tabia ya mtu. Mtume Paulo anasema "Basi vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi ...." Wakolosai 3:5.
UOVU mwingi unakuwa mazoea na tabia ya binadamu kwa sababu ya masikio, tangia utoto unachokisikia ndicho kinakuwa tabia yako, sikio ni kiungo cha pekee kinachokuumbia tabia. Kwa masikio unaweza kujitenga na Mungu na kwa masikio unaweza kuokolewa na kula mema ya nchi
Sikiliza: "Imani chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo" Warumi 10:17. Hebu kila mmoja ajiulize antena za masikio yake zina nasa mawimbi gani? kama ni mawimbi ya music bongo fleva na aina zake, ubongo utajaa hayo na tabia zingine chafu.
Neno la leo linamalizia kwa kusema; "Yeye aligeuzaye sikio lake asiisikie sheria, hata sala yake ni chukizo" Mithali 28:9. Wengi wamejitenga na Muumba wao bila kujua, kwa sababu ya kutosulibisha masikio yao, wakayaacha yanase uchafu, wamejitenga na baraka za Bwana, wamenaswa na adui. Maombi yao yanishia hewani, na hatimaye kukosa matumaini.
Hii ni nafasi nyingine tena ya kila mmoja kutafakari, ni wapi masikio yake yanahitaji matengenezo, Yesu alikufa kwa ajili yetu, huu ni wakati wa kukomboa mateka, na kupatanishwa na Baba yetu. USHINDI NI HAKIKA.
NAWATAKIA SIKU YENYE FURAHA NA BARAKA TELE
Na: Ev. Eliezer Mwangosi
Latest
Previous
Next Post »
Next Post »
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
EmoticonEmoticon