KUOKOLEWA KWA NEEMA

SOMO: MAANA HALISI YA KUOKOLEWA KWA NEEMA
💝👉 Jitahidi ulisome somo lote na ulitafakari. Huu ni wakati wa matengenezo. Pia pata masomo zaidi kupitia -  evmwangosi.blogspot.com 💝

Mtume Paulo anasema: Waefeso 2:8-9 "Kwa maana mmeokolewa kwa NEEMA, kwa njia ya IMANI; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni KIPAWA cha Mungu; wala si kwa MATENDO, mtu awaye yote asije akajisifu".

Hapa tunaona NEEMA ni kipawa cha Mungu, au Zawadi ya wokovu tunayopewa bure bila kulipa chochote. Tunapewa tusichostahili, wala hakuna matendo yoyote tunayopaswa kutenda ili tupewe, hiyo ndiyo tafsiri rahisi ya neno NEEMA.

NEEMA Ndiyo asili ya pekee ya watu kupewa HAKI ya kuwa watoto wa Mungu kwa Imani. Warumi 3:23-24 "Kwa sababu wote wamefanya Dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa HAKI bure kwa NEEMA yake...". Warumi 3:28 "Basi, twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa IMANI pasipo matendo ya sheria".

Kamwe, HAKI ya kuwa wana wa Mungu haipatikani kwa namna yoyote ya sisi kutenda matendo mema, bali inapatikana kwa IMANI juu ya kile alichokifanya Yesu Kristo pale msalabani na kumkubali kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Hata hivyo Imani huzaa MATENDO mema, ndiyo maana neno linasema "Imani bila matendo imekufa" Yakobo 2:17.

Imani iliyo hai inaonekana kwa matendo ya UTII wa SHERIA za Mungu, au maisha matakatifu yasiyo ya Dhambi. Ni wale tu walioguswa na upendo wa Kristo na kubadirishwa maisha yao ndio wanampendeza Mungu wakiishi maisha ya UTII wa sheria bila SHURUTI.

TAFAKARI MFANO HUU:
Kulikuwa na mtu aliyekuwa anaendesha Gari kwa Kasi zaidi ya mwendo ulioonyeshwa kwenye kibao cha alama za barabarani, mbele yake kukawa na mataa (traffic light). Kwa sababu ya mwendo kasi alijikuta amepita mataa yakiwa na rangi nyekundu (RED). Mara baada ya kupita mataa akasimamishwa na Askari, na kupewa adhabu ya kulipa faini ya Sh. 60,000. Kwa makosa mawili, mwendo kasi na kupita mataa na rangi nyekundu.

Bahati mbaya alikuwa hana pesa, akiwa anasubiri kupelekwa kituoa cha polisi kwa ajili ya mashitaka, akatokea mtu mmoja anayemfahamu, akamuonea huruma, na kumlipia faini aliyokuwa anadaiwa. Hatimaye akaachiwa huru na kuendelea na safari yake. Kuanzia pale, katika safari yake yote, aliendelea kukumbuka upendo wa Rafiki yake, na akasukumwa moyoni kuwa mtiifu na mwangalifu kwa Sheria zote za Barabarani, na hakushikwa tena hadi alipofika safari yake.

FIKIRIA: Huyu dereva angerudia kosa la kutojali Sheria za barabarani, angekamatwa tena, na angeonekana Mpuuzi asiye na Akili. Hivyo ndivyo ilivyo Uhusiano kati ya Neema na Sheria. Na NEEMA ya Mungu ni zaidi ya msaada uliotolewa kwenye kisa hicho.

Neema ya Mungu kupitia kafara ya Kristo inafanya mambo makuu matatu yafuatayo:

1. Inatoa msamaha wa Adhabu ya Mauti bure kwa mdhambi, kupitia Mauti ya Kristo msalabani. Kwa sababu mshahara wa dhambi ni mauti. Tukiwa tungali tuna kesi ya kufanya Dhambi, tukingojea adhabu, Yesu Kristo, alijitokeza kutulipia Deni la Dhambi, Wakolosai 2:14. Sasa tuko huru, tunaendelea nasafari.

2. Inatupatanisha na Mungu, na kutupatia HAKI ya kuwa watoto wa Mungu. Kwa dhambi zetu hatukustahili kuitwa watoto wa Mungu wenye kupokea Baraka zake katika ulimwengu huu wa sasa na katika ulimwengu ujao. Katika mwili tulikuwa maadui wa Mungu kwa kutotii Sheria zake - Warumi 8:7.

3. Inatupatia UWEZO wa kutii SHERIA za Mungu kwa njia ya Roho mtakatifu, ambaye huziandika katika mioyo yetu, na kutufanya tuishi maisha matakatifu kwa Imani. Tunatiwa mhuri wa tabia ya Mungu kwa njia ya Roho mtakatifu. Waebrania 10:16 "Hili ni AGANO nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana, nitatia Sheria zangu mioyoni mwao, Na katika nia zao nitaziandika". Tunadumu kusafiri Salaama, bila kunaswa na Traffic, kwa sababu Roho matakatifu ametupatia Utii kuwa tabia.

HITIMISHO:
1. Wale wanaotegemea wokovu kwa matendo mema kwa kutii sheria, bila Kristo kutawala maisha yao kwa Imani, watapotea milele, na wako nje ya WOKOVU halisi.

2. Wale wanaodai wako chini ya NEEMA, huku baadhi ya matendo yao ni kinyume na Sheria au Amri za Mungu, wakisema wako huru kutotii, hao ni vipofu wanahitaji nuru, wamenaswa na walimu wa uongo na mafundisho potofu, wameitiwa UHURU BANDIA, huku wakiasi kwa kujua au kutokujua.

Walio na Imani ya kweli katika Yesu Kristo, wanakuwa chini ya uongozi wa Roho mtakatifu, hao ndio waabuduo halisi, wamwabuduo Mungu katika Roho na Kweli. Hawa wanatembea katika utii wa Amri za Mungu kama Yesu Kristo alivyotii (Hawatendi Dhambi, wameokolewa katika uasi wote) - Yesu anasema; Yohana 15:10 "Mkizishika Amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama mimi nilivyozishika Amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake".

BWANA AZIDI KUBARIKI KILA MMOJA ANAPOFANYA MATENGENEZO YA IMANI.

Na: Ev. Eliezer Mwangosi
Simu: 0766 99 22 65 - Email: eliezer.mwangosi@yahoo.com.
Tovuti: www.mwangosi.com
Previous
Next Post »