KUJIEPUSHA NA LAANA YA TORATI

SOMO: NAMNA YA KUJIEPUSHA NA LAANA YA TORATI
Wagalatia 3:10-14 “Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye. 11- Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani.

12- Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo.13- Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; 14- ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.”

MAANA YA NENO LAANA:
Kwa lugha rahisi neon LAANA lina maana ya Tendo au Tukio Baya linaloweza kumpata mtu kutokana na apizo fulani. Kwa muktadha wa Biblia Laana ni matokeo mabaya katika maisha ya mwanadamu yakiwa ni matokeo ya kutotii maagizo ya Mungu. Kiumbe wa Kwanza kuipata laana kutoka kwa Mungu kwa kutotii ni nyoka, Mwanzo 3:14. Baada ya Anguko la Adam na Hawa, kukatokea makundi mawili, kundi la Uzao wa Nyoka (Wanaomtii Shetani) na Uzao wa Mwanamke (Kristo). Mwanzo 3:15. 2Petro 2:14.

KIINI CHA KUWEPO LAANA
Kama tulivyosoma hapo juu Chanzo cha laana ni KUTOTII au KUASI maagizo ya Mungu au Kutenda Dhambi kulikosababishwa na Shetani kumdanganya Hawa na hatimaye Adam. Baada ya hapo Dhambi iliingia na kuendelea duniani Mfano. Mwanzo 4:6-7 Kaini akaingia kwenye dhambi ya uuwaji na hapohapo Mungu akamuonya na baadaye akapata laana.

LAANA YA TORATI NI NINI?
Laana ya Torati ni Matukio Mabaya katika maisha ya Wana Israeli ambayo Bwana aliwaapiza kwamba wangeyapata endapo wangeshindwa Kutii maagizo yake yote na Amri alizowapatia; Kumbukumbu la Torati 28:15-68, lakini pia wangebarikiwa endapo wangeshika yote aliyowaagiza – Kumb la torati 28:1-14. Hivyo laana ya TORATI ni Mikosi, Balaa, Mauti, Mateso na kila matokeo mabaya ya Dhambi.

HALI YA ISRAELI CHINI YA TORATI
Waesraeli walijitahidi sana kwa nguvu zao kujidhibiti watende kama walivyoagizwa, lakini wengi wao walishindwa, walitumia NGUVU ZA AKILI ZAO na Kujiongezea sheria zingine, napo walishindwa, hawakutambua kuwa wangeweza tu kwa Imani juu ya Mungu. Upofu wao ulikuwa kujitumainia kwa akili zao kuweza KUTII, bila kujenga Imani kwa Mungu. Kumbuka pasipo Imani hakuna kumpendeza Mungu. Paulo anaeleza vizuri kile walichotakiwa kukifanya - Warumi 2:13-27 "... Walishindwa kuishi sawasawa na sheria ambayo ilipaswa wawafundishe mataifa ...".

UJUMBE WA PAULO KWA WAGALATIA
Soma kwa Makini - Wagalatia 6:12-13, Wagalatia 5:6-11, Warumi 26-27 .... Huo Ulikuwa ni ujumbe wa kuwaepusha na elimu ya wayahudi ya kutafuta HAKI kwa matendo ya sharia hasa ya TOHARA, wagalatia walikuwa wanashurutishwa KUTAHIRIWA ili wapokelewe katika kanisa la Kristo. Waliweka TOHARA kuwa njia ya wokovu zaidi ya Kristo, waliotahiriwa walionekana watakatifu hata kama ni wazinifu, wezi, wenye visasi na uovu mwingine, yaani walikuwa wavunja sheria au torati.

KRISTO KUTUKOMBOA NA LAANA YA TORATI
Kristo alikuja kukamilisha mpango wa Ukombozi wa Mwanadamu, kumtoa mwanadamu katika LAANA ya utumwa wa dhambi au UTII KWA SHETANI. Waisraeli walikuwa chini ya LAANA ya TORATI kwa kushindwa kutenda maagizo ya Mungu yaliyo ndani ya Torati. Hata katika siku zetu wengi watakuwa chini ya laana ya torati kwa kutokujua maana halisi ya mafungu hayo ya Mtume Paulo. Hebu soma na kuyatafakari maelezo haya hapa chini ili upate ufahamu zaidi.

Neema ya Kristo inafanya mambo matatu; 1. Inatulipia deni la mshahara wa Dhambi ambao ni MAUTI, tuko HURU na MAUTI, 2. Inatupatanisha na Mungu, kwa kutoa msamaha wa Dhambi Bure tunapewa HAKI ya kuwa watoto wa Mungu, 3. Inatupatia TABIA ya Mungu, inayotuwezesha KUTII Sheria zake bila SHURUTI, hutupatia ushindi na kutufanya watakatifu tusio na mawaa. Warumi 6:1-7, Warumi 5:6-10, Warumi 6:12-18, Warumi 8:3-7.

NB: Kazi kubwa ya NEEMA ya Kristo ni kutufanya sisi watu wa Rohoni tusikumbwe na LAANA ya kuiasi sheria ya Mungu, Neema ipo “ili maagizo ya TORATI yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya Roho” Warumi 8:4. Neema inazifanya Sheria za Mungu ziwe ni TABIA iliyoandikwa moyoni – Waebrania 10:16-17. Katika vizazi vyote HAKI Hupatikana kwa IMANI, Ibrahimu na Manabii wote, akina Eliya, Henoko n.k. Walimwamini na Kumtamainia Mungu, wakashinda UOVU, na kuhesabiwa HAKI kwa Imani, ambayo ilizaa matendo ya UTII wa Sheria zake.

 Kumbuka pia kuwa kuna Sheria zilizoishia Msalabani, zilikamilishwa na Kifo cha yesu, hizo hazihusiani na Sheria za Maadili au Amri za Mungu. Sheria za Kafara za upatanishi, Sheria za kupiga mawe Waasi n.k. Zilikamilishwa msalabani.

JIOKOENI NA KIZAZI HIKI CHA NYOKA:
Wengi wataangamia kwa kukosa Maarifa, jiepusheni na mafundisho ya waalimu walio wa uzao wa Nyoka kizazi cha LAANA, wanaoigeuza KWELI ya Mungu kuwa Uongo, Waipingao Kweli kwa kutolitumia neno la Mungu kwa UHALALI, hao ni Visima vitoavyo matope na bahari iliyochafuka, wawaitiao watu UHURU BANDIA kuwaongoza kumpinga Kristo na kuizidisha LAANA Duniani .. Ufunuo 12:17, Isaya 24:4-6. Marko 7:6-9, Mathayo 5:17-20, Mathayo 7:21-23. Ufunuo 14:12.

PATA MASOMO HAYA KWA UPANA ZAIDI KUPITIA TOVUTI HIZO HAPO CHINI

NEEMA YA MUNGU IKATAWALE MIOYO YENU KUWAANGAZIA NURU YA UTUKUFU WAKE MILELE.

Na: Ev. Eliezer Mwangosi

Email: eliezer.mwangosi@yahoo.com
Simu ya Whatsapp: +255 0766992265
Tovuti: www.mwangosi.com; na blog: evmwangosi.blogspot.com.
Instagram: evmwangosi
Twitter: @EliezerMwangosi
Previous
Next Post »