SOMO LA 2 - NEEMA NA SHERIA

SIKILIZA: INJILI YA MILELE - SEHEMU YA PILI

MADA: UHUSIANO ULIOPO KATI YA NEEMA YA KRISTO NA SHERIA (TORATI) - 2

Somo hili ni muendelezo wa Somo la kwanza, hivyo soma na kulielewa kabla ya Somo hili. Roho mtakatifu atuongoze kuisikia sauti ya Mwokozi kupitia ujumbe huu wa Injili ya Milele.

Kati ya masomo au mada tata anazotumia shetani kuwateka wakristo wengi wasio na maarifa na kuwafanya wamuasi Mungu bila kujua, ni mada hii ya uhusiano wa Neema na Sheria. Katika Somo la kwanza tumepata mambo makuu matatu, ambayo yasipoeleweka vizuri yatafanya wengi wakataliwe siku ya mwisho kama Yesu alivyosema ... Mathayo 7:21-23.

Mambo matatu yanayohitaji maarifa zaidi - 1. Kuokolewa kwa NEEMA, 2. Kuhesabiwa HAKI kwa Imani sio kwa Matendo ya Sheria,  3. Utii wa Amri au Sheria za Mungu. Hebu pitia tena mifano ya mafungu kinzani yafuatayo: Wagalatia 3:10-13 "..Walio wa Matendo ya Sheria wako chini ya LAANA..", Warumi 10:3-4 "..Kristo ni Mwisho wa Sheria (Torati)...", Tazama pia Mathayo 5:17-20 ".. Kristo hakuja kutangua Torati...", 1Yohana 2:4 ".. Yeye asemaye, nimemjua, wala hazishiki Amri zake ni Muongo wala kweli haimo ndani yake". Ufunuo 14:12 "..Watakatifu ni wale wazishikao Amri za Mungu na Imani ya Yesu"... n.k.

Kwa HILA nyingi, ulimwengu umedanganywa na kuingizwa katika UASI mkuu na GIZA NENE la kiroho, shetani ametumia neno SHERIA, TORATI na NEEMA vibaya, na hatimaye dunia kujaa laana kama Isaya alivyotabiri, Isaya 24:4-6, 19-20 "... Kwa kuasi SHERIA za Bwana dunia IMELAANIWA na mzigo wa Dhambi umeilemea na inaenda kuanguka...".

Kwanza kabisa tuangalie utata uliopo kwenye neno lenyewe SHERIA au TORATI, na kujibu maswali yafuatayo; Neno TORATI lina maana gani? Je Amri za Mungu ambazo usipotii unaitwa Mdhambi ndio Torati? Torati imeanza na Ililetwa lini? Mungu aliitoa kwa makusudi gani? Je sisi tulio okolewa kwa Neema Yesu inatuhusu kwa namna yoyote?

MAANA YA NENO TORATI:
Kwa lugha ya asili,  TORATI maana yake ni SHERIA Ambayo ndani yake ina; MAUSIA, SHERIA, AMRI, HUKUMU, SHUHUDA - Soma 1Wafalme 2:3-4 "Uyashike mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia Zake, uzishike Sheria Zake, na Amri Zake, na Hukumu Zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika TORATI ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo na kila utazamako. Kwa tafsiri ya kawaida Torati (Torah) ni Muongozo (Instruction or Guidance).

Kwa muktadha wa Biblia na wayahudi walivyoamini, Torati ni Vitabu vitano 5, vilivyoandikwa na Musa - Mwanzo, Kutoka, Mambo ya walawi, Hesabu na Kumbukumbu la Torati. Kwa Wayahudi ukisema Torati maana yake ni maandishi yote ya Musa aliyoyaandika kutoka kwa Bwana. Wayahudi walitengeneza Sheria 613, kutoka katika Vitabu vitano vya Musa, kwa ajili ya msistizo na urahisi wa kufundisha.

Sheria hizo 613 ziligawanywa katika Vitabu 31 kutokana na matumizi - Mfano: Utii kwa Mungu, Utakaso, Usafi, Vita, Wafalame, Hukumu na Adhabu, Huduma za Hekalu, Kafara, Mashamba, Mavuno, Familia, Vyakula, Biashara na mikopo, Sikukuu n.k. Unaweza kuzihakikisha kupitia tovuti hii: "http://therefinersfire.org/original_commandments1.htm". Unaweza pia kupata maelezo zaidi kupitia tovuti zingine, tafuta - 613 Laws.  Mbali na hizo zilizoandikwa, walikuwa nyongeza ambazo hazikuandikwa bali zilikuwa zinarithiwa kwa mdomo.

Zingatia:
Kiuandishi Torati inajumuisha sheria za aina mbili, ya Kwanza ni - Amri au Sheria inayoonyesha Dhambi, kwa muhtasari ziko AMRI 10 - Kwanza zilipotolewa kwa Musa, ziliandikwa na Mungu mwenyewe juu ya mawe "Kutoka 31:18", zilikuwa zinatunzwa ndani ya Sanduku la Agano - "Kumbukumbu la torati 10:5", Ni za milele, Takatifu na kamilifu "Warumi 7:12, Zaburi 111:7-8, Mathayo 5:17-19, Zaburi 19:7", Ndio jumla ya Mapenzi ya Mungu ambayo inampasa mwanadamu kutenda "Mhubiri 12:13, Yakobo 2:10-12". Kutozitii ndio UASI au DHAMBI.

Sehemu ya Pili - ndio inayojumuisha Sheria zingine zote zilizobaki, pamoja na hukumu, maagizo, mashauri n.k. Hizi ziliandikwa "Kutoka 31:19", Ilitunzwa nje ya Sanduku "Kum la Torati 31:26", Baadhi ziliondolewa, zilikuwa kivuli au mfano katika mpango wa ukombozi "Waebrani 9:10-11, Waefeso 2:15". Pia zingine hatulazimiki kuzishika kiroho kutokana na mfumo wa jamii, mfano - Sheria za vita, mahakama, Tohara, Kusaza mavuno, kuwaua waovu, riba za mikopo. nk. Ingawa kuna Sheria nyingi bado jamii inazitumia hata katika serikali zetu, mfano. Sheria za Afya, kupumzisha mashamba, sheria za mahakama, mirathi na wajane nk.

Katika Somo litakalofuata tutaangali kwa undani chanzo cha TORATI au SHERIA na sababu zilizomfanya Mungu aitoe kwa wanadamu.

Na: Ev. Eliezer Mwangosi
Simu: 0767 210 299 - Kwa ajili ya maswali, ushauri na Maombi kwa wenye Shida.

Previous
Next Post »