SIKILIZA: INJILI YA MILELE - SEHEMU YA KWAZA
MADA: UHUSIANO ULIOPO KATI YA NEEMA YA KRISTO NA SHERIA (TORATI) - 1.
Kumekuwa na majadala mkali juu ya Kushika Sheria (TORATI), baada ya kuokolewa yaani kuwa chini ya Neema ya Kristo. Utata uliopo unatokana na baadhi ya mafungu ya biblia yanayohitaji ufahamu mpana, ili kuelewa bila kupotosha lengo la mwandishi. Wengi wametumia nyaraka za mtume Paulo kupotosha ukweli wa Injili kama mtume Petro alivyotoa tahadhari. 2Petro 3:15-17.
Kuna mafungu yanayoonyesha kutohitajika Sheria au Torati baada Kristo ... Mfano: Wagalatia 3:10-13 "..Walio wa matendo ya Sheria wako chini ya LAANA.... Kristo alitukomboa katika LAANA ya TORATI...", Wagalatia 3:19 "..TORATI iliingizwa kwa sababu ya Makosa....", Warumi 10:3-4 "...Kristo ni mwisho wa Sheria..", Warumi 3:23-25 "...Torati ni kiongozi kutuleta kwa Kristo..... Hatupo tena chini ya Kiongozi....", Wakolosai 2:16 "Basi mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya mwandamo wa mwezi, au sabato....".
Wagalatia 5:1-4 "..Msinaswe tena chini ya Kongwa la Utumwa.... Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa Sheria; Mmeanguka na kutoka katika hali ya Neema". Yapo mafungu mengine mengi yanayokinzana na sheria, japo nimeyachukuwa kama mfano. Ukiyasoma mafungu hayo kijujuu utaona yanapinga kabisa kuwepo au kujifunza Sheria ya Mungu.
Kwa Upande mwingine, tunamuona mtume Paulo na hata Kristo mwenyewe akionyesha umuhimu wa Kujifunza na kutenda sawa sawa na Sheria, kwa Mfano: Ujumbe kwa Warumi, Warumi 2:12-13 "...Kwa sababu sio wasikiao Sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao Sheria watakaohesabiwa HAKI".
Warumi 7:7-12 ".... Torati au Sheria ndiyo inayoonyehsa dhambi... TORATI ni Takatifu, na ile AMRI ni takatifu, na ya Haki na Njema...", Warumi 7:14 "...Torati asili yake ni Rohoni...". Warumi 8:3-8 "...Kristo alikuja ili maagizo ya Torati yatimizwe ndani yetu sisi....Kwa kuwa ile nia ya mwili ni UADUI juu ya Mungu, kwa maana haitii SHERIA ya Mungu, wala haiwezi Kuitii".
Yesu alisisitiza kabisa juu ya kuzishika Sheria au Amri za Mungu ... Yohana 15:10 "Mkizishika Amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika Amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake", Mathayo 5:17-20 "...Yesu hakuja kutangua Torati wala Manabii, bali kutimiliza..." Anatimiliza kwa kuangazia mioyo yetu Sheria za Mungu kama tabia ya Mungu ya Upendo. Ufunuo 14:12 "Hapa ndipo penye Subira ya Watakatifu, hao wazishikao Amri za Mungu, na Imani ya Yesu".
Yesu haleti Sheria mpya, bali anazifafanua na kuzipatia nafasi katika mioyo yetu kuwa sehemu ya tabia kwa njia ya Imani - Mtume paulo anasema; Waebrania 10:16-17 "...anena Bwana, Nitatia Sheria zangu mioyoni mwao, na katika nia zao nitaziandika....Ndipo... Dhambi zao na Uasi wao sitaukumbuka tena kabisa". Huo, ndio wokovu halisi, uhuru mbali na dhambi, Kuwa watii wa sheria za Mungu bila kuogopa adhabu.
Kutokana na maelezo yote, hapo juu bado, kuna maswali mengi ambayo yanahitaji maelezo ... Kwa Mfano; Je tunapaswa kushika Sheria zote za Torati? Torati maana yake nini, nini kishikwe na nini kiachwe ndani ya Torati baada ya Kristo? Nini Kazi ya neema juu ya Sheria? Kwa nini Mungu awapatie watu TORATI ambayo baadaye inaitwa laana? Alikuwa na makusudi gani kuwapatia watu mzigo usiwezekana kuubeba? Yesu anaposema Amri mpya nawapa anamaanisha nini? n.k.
Usikose Kupata majibu, katika mfululizo wa uchambuzi wa Mada hizi tata, ambazo Adui anazitumia kuwapoteza wengi kupitia walimu wasio na ufahamu, na hatimaye kuisabibishia dunia nzima kuingia kwenye laana ya kutisha kabla ya kuangamizwa kwa sababu ya UASI. Isaya 24:4-6.
MUNGU AWABARIKI WOTE, KARIBUNI KWA SOMO LA 2 LITAKALOFUATA.
Wenu: Ev. Eliezer Mwangosi
Simu: 0767 210 299. Kwa ajili ya Maswali, Ushauri na Maombi.
1 comments:
Write commentsMkristo anatakiwa kuishi kwa sheria ya uhuru (Imani itendayo kazi kwa upendo) sio Torati.Yak 1:25, 2:8-9 Gal 5:6, 13
ReplyEmoticonEmoticon