SOMO LA 4 - NEEMA NA SHERIA

SIKILIZA: INJILI YA MILELE - SEHEMU YA NNE

MADA: UHUSIANO ULIOPO KATI YA NEEMA YA KRISTO NA SHERIA - 4

Karibuni katika mfululizo wa Mada hii ya Uhusiano kati ya NEEMA na SHERIA. Somo hili ni la 4, ni imani yangu kuwa, ulishasoma na kutafakari somo la 1 hadi 3, kama bado jitahidi kuyasoma masomo hayo kabla ya kuanza kujifunza somo hili. Masomo haya ni ya muhimu sana kwa kila Mkristo aliyezaliwa mara ya pili na kutarajia kuurithi uzima wa milele.

Zingatia: Katika somo hili, tunajifunza juu ya uhusiano uliopo kati ya NEEMA na Sheria za Maadili (Amri za Mungu) zinzoonyesha Dhambi, tofauti na sheria zile zingine zikiwemo zilizokuwa kivuli cha Kristo na kukamilishwa au kuishia pale msalabani.

MAANA YA NEEMA.
Mtume Paulo anasema: Waefeso 2:8-9 "Kwa maana mmeokolewa kwa NEEMA, kwa njia ya IMANI; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni KIPAWA cha Mungu; wala si kwa MATENDO, mtu awaye yote asije akajisifu". Hapa tunaona NEEMA ni kipawa cha Mungu, au Zawadi ya wokovu tunayopewa bure bila kulipa chochote. Tunapewa tusichostahili, wala hakuna matendo yoyote tunayopaswa kutenda ili tupewe.

NEEMA Ndiyo asili ya pekee ya watu kupewa HAKI ya kuwa watoto wa Mungu kwa Imani. Warumi 3:23-24 "Kwa sababu wote wamefanya Dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa HAKI bure kwa NEEMA yake...". Kama ndivyo; AMRI au Sheria zina Kazi gani? Kuna haja gani ya kuzitii?

TAFAKARI MFANO HUU:
Kulikuwa na mtu aliyekuwa anaendesha Gari kwa Kasi zaidi ya mwendo ulioonyeshwa kwenye kibao cha alama za barabarani, mbele yake kukawa na mataa (traffic light). Kwa sababu ya mwendo kasi alijikuta amepita mataa yakiwa na rangi nyekundu (RED). Mara baada ya kupita mataa akasimamishwa na Askari, na kupewa adhabu ya kulipa faini ya Sh. 60,000. Kwa makosa mawili, mwendo kasi na kupita mataa na rangi nyekundu.

Bahati mbaya alikuwa hana pesa, akiwa anasubiri kupelekwa kituoa cha polisi kwa ajili ya mashitaka, akatokea mtu mmoja anayemfahamu, akamuonea huruma, na kumlipia faini aliyokuwa anadaiwa. Hatimaye akaachiwa huru na kuendelea na safari yake. Kuanzia pale, katika safari yake yote, aliendelea kukumbuka upendo wa Rafiki yake, na akasukumwa moyoni kuwa mtiifu na mwangalifu kwa Sheria zote za Barabarani, na hakushikwa tena hadi alipofika safari yake.

FIKIRIA: Huyu dereva angerudia kosa la kutojali Sheria za barabarani, angekamatwa tena, na angeonekana Mpuuzi asiye na Akili. Hivyo ndivyo ilivyo Uhusiano kati ya Neema na Sheria. Na NEEMA ya Mungu ni zaidi ya msaada uliotolewa kwenye kisa hicho.

Neema ya Mungu kupitia kafara ya Kristo inafanya mambo makuu matatu yafuatayo:
1. Inatoa msamaha wa Adhabu ya Mauti bure kwa mdhambi, kupitia Mauti ya Kristo msalabani. Kwa sababu mshahara wa dhambi ni mauti. Tukiwa tungali tuna kesi ya kufanya Dhambi, tukingojea adhabu, Yesu Kristo, alijitokeza kutulipia Deni la Dhambi, Wakolosai 2:14. Sasa tuko huru, tunaendelea nasafari.

2. Inatupatanisha na Mungu, na kutupatia HAKI ya kuwa watoto wa Mungu. Kwa dhambi zetu hatukustahili kuitwa watoto wa Mungu wenye kupokea Baraka zake katika ulimwengu huu wa sasa na katika ulimwengu ujao. Katika mwili tulikuwa maadui wa Mungu kwa kutotii Sheria zake - Warumi 8:7.

3. Inatupatia UWEZO wa kutii SHERIA za Mungu kwa njia ya Roho mtakatifu, ambaye huziandika katika mioyo yetu, na kutufanya tuishi maisha matakatifu kwa Imani. Tunatiwa mhuri wa tabia ya Mungu kwa njia ya Roho mtakatifu. Waebrania 10:16 "Hili ni AGANO nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana, nitatia Sheria zangu mioyoni mwao, Na katika nia zao nitaziandika". Tunadumu kusafiri Salaama, bila kunaswa na Traffic, kwa sababu Roho matakatifu ametupatia Utii kuwa tabia.

HITIMISHO:
Kamwe mwanadamu hawezi kuhesabiwa haki kwa matendo ya Sheria. Wagalatia 2:16 "Hali tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi HAKI kwa kwa matendo ya Sheria, bali kwa Imani ya Kristo Yesu; sisi tulimwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe haki kwa Imani ya Kristo, wala kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki". Leo kuna wengi watapotea kwa kutegemea matendo yao mema, yasiyo matokeo ya kubadirishwa na kuongozwa na Roho mtakatifu, na wengine aanakataa na kupinga WOKOVU katika Kristo, Watapotea bila matumaini.

Walio na Imani ya kweli katika Yesu Kristo, wanakuwa chini ya uongozi wa Roho mtakatifu, hao ndio waabuduo halisi, wamwabuduo Mungu katika Roho na Kweli. Hawa wanatembea katika utii wa Amri za Mungu kama Yesu Kristo alivyotii (Hawatendi Dhambi au UASI) - Yesu anasema; Yohana 15:10 "Mkizishika Amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama mimi nilivyozishika Amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake". Yakobo anasema "...Imani pasipo MATENDO imekufa" Yakobo 2:26.

Wale wote, wanaodai wako chini ya Neema, wakidai wako huru na Sheria, na kutotaka hata kusikia Sheria ya Mungu, watapotea milele. Kuchukia Amri za Mungu ni tabia ya yule Adui Joka kwa Kanisa la Kristo - Ufunuo 12:17 "Joka akamkasirikia yule mwanamke (Kanisa), akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao Amri za Mungu, na kuwa na Ushuhuda wa Yesu.....". Shetani, amelitumia somo hili la Neema na Sheria kuwapofusha wengi, wasiopenda kuisikia kweli ya Mungu na kuzigeukia hadithi za Uongo. Tunaishi nyakati mbaya zilizotabiriwa za Ukengeufu mkuu - heri wewe usomaye ujumbe huu na kuufanyia kazi. 2Timotheo 4:3-4, 2Petro 3:14-18.

Mungu awabariki wote, mnapoendelea kutafakari ujumbe huu wa Injili ya Milele, yenye wito wa Kumcha Mungu katika kizazi hiki kilichojaa uovu, na mioyo mikaidi isiyotaka kumtii Mungu. Usikose somo la 5, linalohusu kukamilishwa kwa Upendo wa Mungu kupitia NEEMA.

NAWATAKIA SIKU NJEMA YENYE BARAKA TELE

Na: Ev. Eliezer Mwangosi
Simu: 0767 210 299 - Email: eliezer.mwangosi@yahoo.com.

Wapelekee pia wengine ujumbe huu wa matengenezo.

Previous
Next Post »