SIKILIZA: INJILI YA MILELE - SEHEMU YA TATU
MADA: UHUSIANO ULIOPO KATI YA NEEMA YA KRISTO NA SHERIA (TORATI) - 3
Somo hili ni muendelezo wa Somo la pili, hivyo unashauriwa kusoma na kuelewa masomo yaliyotangulia kabla ya Somo hili. Roho mtakatifu atuongoze kuisikia sauti ya Mwokozi kupitia ujumbe huu.
Kumbuka; kwa kutoelewa vizuri somo hili la uhusiano wa Neema na Sheria, unaweza kuwa kati ya watu walio katika LAANA kwa kutaka kuhesabiwa haki kwa matendo ya sheria (Torati) kama mtume Paulo alivyosema - Wagalatia3:10-13. Au ukawa upande wa pili wa watakao hukumiwa kwa UASI wa Amri (SHERIA) za Mungu, yaani upande wa waovu walio mbali na wokovu - 1Yohana 2:4, Zaburi 119:155. Ni wakati wa kuzifunua HILA ZA SHETANI NA KUZIPINGA.
Katika somo lililopita tumeona ndani ya neno TORATI (SHERIA) kuna mgawanyiko wa aina za sheria, aina ya kwanza ni AMRI, ambazo zinaonyesha tabia au maadili (MORAL LAW ) au Mapenzi ya Mungu, mwanadamu asipotii anakuwa AMEASI au ametenda DHAMBI. Aina ya pili ya Sheria inajulikana kama sheria za maagizo, wakati mwingine zinaitwa sheria za Musa. Katika somo hili tutaangalia, lini Torati ilianza, na makusudi ya Mungu kuitoa torati kwa mwanadamu.
TORATI ILIANZA LINI?
Kutokana na maelezo hayo hapo juu, Baadhi ya Sheria au Torati ilianza tangia Mwanzo Kabla ya Musa au Taifa la Isareli. Yaani, mapenzi ya Mungu yalikuwepo na yatadumu kuwepo MILELE ndio maana Dhambi inadumu hadi leo. Kizazi cha Nuhu, bila kusahau Sodoma na Gomora waliangamizwa kwa sababu ya kutotii Sheria za Mungu Kabla ya Taifa la Israeli kuwepo na kabla ya torati kutolewa tena kwa Musa. Mfano - Mwanzo 4:7, Mwanzo 13:13, Mwanzo 6:5-8, Sheria ya kafara Mwanzo 22:13.
KWA NINI MUNGU ALIMPATIA TENA MUSA TORATI?
1. Kuwakumbusha Mapenzi yake au Sheria zake ambazo waisareli walizisahau wakiwa Utumwani Misri, ili wasimtende Dhambi. Ambazo kuanzia Mwanzo kwa Adam, kizazi cha Nuhu, hadi Ibrahimu baba yao alizishika kwa Imani na kuhesabiwa haki Kabla yao. Sheria ya Milele aliiandika katika vipande vya mawe, kwa ufupi zikiwa 10, ambazo baadaye Yesu alizifundisha kwa Mapana akieleza namna ya kuzitenda.
Mathayo 5:19-20.
2. Kuwafundisha namna ya kuishi ili wafanikiwe, kiroho na kimwili, kama taifa lenye jamii isiyo kuwa na, Utawala wenye mamlaka, wala Madaktari na Bwana afya, wala vikosi vya maskari wa vita na ulinzi, wala wanasheria na mahakimu, wasio na washauri wa ndoa, wala wataalamu wa biashara na mikopo, hakuwa na Mabwana shamba n.k. Mungu aliamua kuwapatia kanuni zote za maisha ili kuwafanikisha katika maisha yao. Hivyo kanuni zote na maagizo ya Torati kwa waisraeli yalitolewa kwa sababu ya Upendo wa Mungu kwa watu wake wapate kufanikiwa. Yoshua 1:7-8.
3. Katika pambano kuu kati ya Wema na Ubaya, Mungu aliweka Mpango wa Ukombozi kwa wanadamu walioanguka dhambini, Kabla ya Yesu kuja; Mungu alitoa sheria zilizokuwa zinalenga kifo cha Yesu msalabani, kulikuwa na sheria za huduma za Kafara na Upataniso. Hizi ziliambatana na vyakula, vinywaji, miandamo ya miezi. Siku zilipokuwa zikifanywa ilikuwa ni Mapumziko rasmi (Sabato), Mfano soma: Mambo ya walawi 4:26-29, 16:5-30, 23:26-38, 25:8-10 pia Hosea 2:11 nk. Sheria zote za huduma za kafara na upatanisho, ZILIKAMILISHWA na kifo cha Yesu pale msalabani.
Jambo la Msingi kufahamu ambalo Shetani hataki likae katika akili zetu ni hili; Mungu ni PENDO na kwamba wakati wote anatuwazia mema ili tufanikiwe, Torati au Sheria zimetolewa na Mungu ili mwanadamu, kwa nyakati tofauti, apate kufanikiwa katika nyanja zote. 1Wafalme 2:3-4. Tukijua hilo, tutakuwa na hekima ya kujua lipi ni hitaji letu kwa sasa ili tufanikiwe kiroho na kimwili na lipi halitakiwi kwa sasa kutokana na Neno la Mungu.
ZINGATIA:
Mungu ni Upendo - 1Yohana 4:8, 16. Mungu wakati wote hutuwazia mema ili tufanikiwe - Yeremia 29:11, 33:9. Mungu hana kigeugeu - Malaki 3:6, wala hawezi kusema uongo - Hesabu 23:19. Hivyo hawezi kutoa sheria zenye kudhuru maisha mwanadamu, halafu ajutie na kufanya marekebisho. Ndio maana mtume Paulo anasema Torati asili yake ni ya Rohoni. Na Yesu alikuja ili Torati itimizwe ndani yetu kwa Imani - Warumi 8:3-4.
Mungu awabariki mnapoendelea kutafakari ujumbe huu, japo unaweza kuwa na maelezo kwa kifupi juu ya Torati - Somo la NNE, tutaanza kujifunza Kazi ya Neema juu ya Amri au Sheria za Milele, zinazoonyesha mapenzi ya Mungu na Uovu (DHAMBI). Pia tutajifunza maana ya Yesu kuja KUTIMILIZA Torati na Manabii - Mathayo 5:17-20.
WEMA WA MUNGU UENDELEE KUWA JUU YA KILA MMOJA ANAYEHITAJI KUNYWA MAZIWA YASIYOGHOSHIWA.
Na: Ev. Eliezer Mwangosi
Simu: 0767 210 299 - Kwa ajili ya maswali, ushauri na Maombi kwa wenye Shida.
Next
« Prev Post
« Prev Post
Previous
Next Post »
Next Post »
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
EmoticonEmoticon