MSAMAHA WA DHAMBI

SOMO: MSAMAHA WA DHAMBI

➡ Hili ni moja kati ya masomo muhimu sana katika mfululizo wa masomo haya. Katika somo hili tutagundua upendo mkuu wa ajabu, wingi wa rehema na neema za Mungu. Somo hili ni la kipekee kwa sababu lina muhusu kila mmoja wetu. Je, ni nani ambaye hana dhambi ambaye hahitaji rehema za Mwenyezi Mungu? Kwa hakika somo hili lina mambo muhimu ya kutafakari.

I. Hali Ilivyokuwa Kabla ya Dhambi
➡ Kabla hatujatafakari juu ya mpango wa Mungu wa kusamehe dhambi  tuangalie kwanza hali ilivyokuwa kabla ya dhambi. Dunia hii ilipoumbwa ilikuwa nzuri ajabu, mito ilikuwa mitulivu, maua na mimea viliipamba vizuri, kila kitu kilikuwa katika ulinganifu kabisa. Hakukuwa na matetemeko, majani hayakukauka, wala jani halikudondoka, hakuna kilichopoteza uhai – dunia ilipendeza sana. Wanadamu walikuwa na mahusiano ya amani na furaha na viumbe vyote. Mungu alikuwa ameviumbe viumbe vyote kwa ukamilifu wote. Hakukuwa na kilema, wala ugonjwa, hakukuwa na njaa, vifo wala huzuni. (Mwanzo 1-2).
➡ Mara kwa mara Mungu aliwatembelea Adamu na Hawa, ilikuwa ni furaha na amani siku zote.  (Mwanzo 3:8). Mahali hapa ndipo Mungu alikuwa amempangia mwanadamu aishi.

II. Hali Ilivyo Baada ya Dhambi
➡ Baada ya kuanguka dhambini, jamii yote ya wanadamu walikabiliwa na laana ya kifo na kupotea milele (Warumi6:23). Dhambi ni kuwa kinyume dhidi ya MUNGU, ni kujitenga mbali na chanzo cha uzima - dhambi inafisha.

III. Mpango wa Wokovu
➡ Hata kabla ya kumwumba, Mungu alijua kuwa mwanadamu angeasi. Hata hivyo, hakuacha kumwumba bali aliamua kuandaa mpango wa kumkomboa kutoka katika laana hii ya dhambi – kifo cha milele (Ufunuo 13:8).

➡ Kulingana na maandiko "mshahara wa dhambi ni mauti" (Warumi 6:23) nayo dhambi yaweza kuondolewa tu kwa damu kumwagika. Huu ndiyo utaratibu wa kuondoa dhambi uliowekwa na Mungu. Hii inatupatia picha  ya uzito wa ubaya wa dhambi lakini pia gharama yake. Waebrania 9:22 “Naam, kadiri ya sheria karibu kila kitu chaweza kutakaswa kwa damu, na dhambi nazo zaondolewa tu ikiwa damu imemwagwa.” (Toleo la Kiswahili cha Kisasa). Soma pia Walawi 17:11.

➡ Maandiko yanasema kuwa msamaha wa dhambi (ukombozi wa wanadamu) unapatikana tu katika Kristo Yesu. Warumi 3:23-25 inasema: “Kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho”

Katika Ufunuo 1:5imeandikwa pia kuwa: “Yeye (Yesu) atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake,”

➡ Hebu tafakari pia aya hii ya Quran Tukufu. Quran 19:21: “(Malaika) akasema: … Na ili tumfanye (Isa bin Marryam) kuwa ni ufunuo kwa watu, na Rehema itokayo kwetu, ...” Aya hii inasema rehema (msamaha wa dhambi) toka kwa Mwenyezi Mungu imekuja kupitia katika Isa bin Marryamu yaani Yesu Kristo. Vitabu vyote hivi vifundisha juu ya wokovu wa wanadamu kupitia katika Kristo Yesu. Yesu kama mwokozi wa wanadamu.

IV. Hakuna Msamaha kwa Njia Nyingine
➡ Katika Matendo 4:12imeandikwa: “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.” Na Yesu mwenyewe alisema “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi” Yohana 14:6

V. Kazi Anayofanya Sasa Yesu Mbinguni
➡ Baada ya kukamilisha mpango huu wa ukombozi kwa kumwaga damu yake juu ya msalaba, Yesu anafanya kazi ya kuwapatanisha na Mungu wale wote wanaotubu na kuacha njia zao mbaya.

➡ Maandiko yanasema Yesu ni Kuhani wetu mkuu (Waebrania 9:11). Kazi anayofanya sasa ni pamoja na kuwaombea msamaha kwa Mungu Baba wale wote wanaokubali kutubu na kuacha dhambi. Katika 1Yohana 2:1-2 imeandikwa  “Watoto wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu … tena ndiye anayetuombea”. Somo hili linatufundisha pia kuwa Yesu pekee ndiye mwombezi wetu. Kulingana na maandiko yeye peke yake, kama kuhani, ndiye mwenye majukumu ya kuwaombea wanadamu. Yeye peke yake.

VI. HITIMISHO
➡ Ikiwa mtu ana ugonjwa wa kufisha lakini hatambui tatizo lake au kutafuta tiba sahihi, hakika mtu huyo atakufa! Hiyo ndiyo hatima ya wanadamu wote wanaoshindwa kutambua hali yao ya kiroho na hawatafuti tiba sahihi ya dhambi zao - damu ya Yesu..
➡ Maandiko yanasema kuwa hiki ni kipindi cha rehema. Kipindi ambacho Yesu bado anafanya kazi ya kuwapatanisha wanadamu na Mungu wao. Nataka nikwambie mpendwa kuwa,  kulingana na maandiko, kipindi hiki hakitaendelea milele zote. Maandiko yanasema kuwa, hivi karibuni Mungu atafunga huduma hii ya kusamehe dhambi. Akifunga huduma hii Yesu atasema "imekwisha, mwenye dhambi na aendelee kuwa na dhambi zake" (Ufunuo 22:11). Wakati huo wale wote ambao hawatakuwa wamesalimisha maisha yao,  ambao hawatakuwa wametubu na kuacha dhambi  haitawezekana tena kabisa kusamehewa dhambi zao. Hakika wataangamia milele zote katika uovu wao kwa sababu hawakutaka kuuacha.  Hiki ni kipindi ambacho Mungu anaendelea kutoa wito kwa wote wenye mwili, anawasihi sana sana waache dhambi zao wasahihishe njia zao zilizopinda wapate kuokolewa. Hatujui ni lini rehema hizi zitakoma lakini pia hatujui maisha yetu yatakoma lini. Tunapaswa kujipatanisha na Mungu wetu wakati wote.

MUNGU AKUBARIKI SANA UNAPOTAFAKARI SOMO HILI


Previous
Next Post »