SOMO: DINI YA KWELI YA MWENYEZI MUNGU
1. Dini Ni Nini?
Dini ni imani katika na ibada kwa mamlaka yenye uwezo wa juu kupita wa kibinadamu hususa ni Mungu au miungu.
2. Dini na Makanisa Ulimwenguni
➡ Kama tulivyokwisha kuona huko nyuma takwimu zinaonyesha kuwa duniani kote kuna aina za dini zipatazo 4,200. Kuna Ukristo, Uislam, Ubudha, Uhindu, Umamoni, Uyahudi, Tao, Rastafarian, Baha’I, Umizimu, Shinto, Upagani n.k mpaka takribani dini 4200 (Wikipedia Encyclopedia). Tuliona pia katika dini hizi kuna madhehebu mbali mbali: Kuna madhehebu ya Kikristo zaidi ya 41,000 (World Christian Encyclopedia). Ingawa kila dini na kila dhehebu linajiona kuwa liko sahihi na kwamba linaelekeza watu katika njia ya kweli, Mungu anatambua dini (imani) moja tu. Maandiko yanasema; “Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja” Efeso 4:5. Kuna kanisa moja tu la Mungu (1 Wakorintho 15:9, Ufunuo 2:9). Si mapenzi ya Mungu kuwa na utitiri wa dini na imani, bali anatamani watu wote wawe na imani inayofuata taratibu zake (Yohana 17: 17, 21, 22; 1Wakorintho 1:10).
3. Sifa za Dini ya Kweli
➡ Maandiko yanasema; “Na waende kwa sheria na ushuhuda; ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi.” Isaya 8:20. Katika Quran 42:12, 13 imeandikwa kuwa Muhammad aliagizwa: ”... Bila shaka Yeye (Mola( ndiye Ajuaye kila kitu. Amekupeni sharia ya Dini ile ile Aliyomuusia Nuhu na Tuliyokufunulia wewe na tuliyomfunulia Ibrahim, na Musa na Isa kwamba simamisheni Dini wala msifarikiane kwayo kwa ajili ya Dini; ...( Aya hizi zinasema dini ya kweli inatunza sheria za Mungu na kumshuhudia Kristo kama Bwana na Mwokozi.
4. Dini ya Kweli Kabla ya Taifa la Israeli
➡ Tangu mwanzo wazee wa imani walitii amri na sheria za Mungu: kuanzia kwa Adamu – Nuhu – Ibrahim n.k. Wote walijua kuwa hii ndiyo iwapasayo watu wote (Mhubiri 12:13). Katika habari ya Ibrahimu, aliye baba wa imani, imeandikwa; “Kwa sababu Ibrahimu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na amri zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu” Mwanzo 26:5.
5. Dini ya Kweli Katika Israeli
➡ Maandiko yanaonyesha kuwa Mungu aliwapa Israeli amri 10, mfumo wa ukuhani, hema ya ibada ili kuwafanya wawe na maisha ambayo yangedhihirisha kwamba wao ni watu wa Mungu kweli kweli na vitu hivyo viwaongoze katika lengo hilo (Kutoka 19 – 20).
6. Dini ya Kweli Wakati wa Yesu.
➡ Yesu aliye kiongozi wetu mkuu alisema; "Msidhani ya kuwa nimekuja kutangua Sheria na mafundisho ya manabii. Sikuja kutangua bali kukamilisha” Mathayo 5:17-19. Anasema amri za Mungu ni za milele na kwamba; “Mkinipenda, mtazishika amri zangu” Yohana 14:15.
7. Dini na Kanisa la Kweli Kabla ya Marejeo ya Yesu Mara ya Pili.
➡ Maandiko yanasema wakati wanasubiri Yesu kurudi mara ya pili watu wa Mungu wataendelea kutunza amri zake na kuwa na imani ya Yesu. Imeandikwa; “Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu” Yohana 14:12. Katika ukurasa wa mwisho wa biblia, Mungu anasema “Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake” Yohana 22:14. Katika toleo la King James Version fungu hili linasomeka “Blessed are they that do his commandments …”. Hii ni sawa na kusema “Heri hao wazishikao amri (za Mungu) …”.
8. Sifa za Dini za Uongo
➡ Akiongelea juu ya dini za uongo Mungu anasema; “Makuhani wake wameihalifu sheria yangu, wametia unajisi vitu vyangu vitakatifu; hawakuweka tofauti ya vitu vitakatifu na vitu vya kutumiwa sikuzote; wala hawakuwafundisha watu kupambanua vitu vichafu na vitu vilivyo safi, nao wamefumba macho yao, wasiziangalie sabato zangu, nami nimetiwa unajisi kati yao” Ezekilei 22:26. Aya hii inasema mfumo wowote wa dini unaofundisha tofauti au kipindisha amri na maagizo ya Mungu ni wa uongo.
➡ Nabii Danieli, Yesu Kristo, Mtume Paulo, Mtume Yohana walitabiri kuinuka kwa uasi katika dini na makanisa (Matendo 20:29-30, Mathayo 24:24). Nabii Danieli alitabiri kuinuka kwa mamlaka ya kidini ambayo ingebadili sheria za Mungu. Danieli 7:25 “… ataazimu kubadili majira na sheria.” Kama ilivyotabiriwa; mamlaka hii imefanikiwa kuuangusha ukweli hata chini na inatenda inavyopenda yenyewe (Danieli 8:12; Ufunuo 13:5). Kati ya sheria/ amri zilizoangushwa ni amri ya pili inayozuia matumizi ya sanamu katika ibada (Kutoka 20:4-6), amri ya nne inayowaamru watu wote kupumzika siku ya sabato takatifu ya Mungu, siku ya Jumamosi (Kutoka 20:8-11). Mamlaka hizi zimepotoa pia mafundisho mengine mengi ya Mungu ikiwa ni pamoja na kuanzisha ubatizo bandia, ibada za wafu ambazo ni machukizo mbele za Mungu (Kumbukumbu 18:10-12).
9. Hitimisho
➡ Kwa zaidi ya mwezi maandiko yamefunuliwa nayo yameweka bayana kati ya ukweli na uongo; kati ya mafundisho ya Mungu na yale yaliyotungwa na wanadamu. Kwa huruma nyingi, Mungu ameendelea kuwaita watu watoke katika imani za uongo kabla hajaiangamiza dunia hii. Mungu ameruhusu nuru hii ikufikie ili ufanye uchaguzi ukiwa unajua; uchaguzi wa aidha kufuata ukweli au uongo, uzima au mauti. Jambo moja sasa ni hakika nuru hii itakuwa aidha ushuhuda siku ya hukumu yako au itakuwa wokovu kwako. Ukiikataa nuru hii Mungu anasema naye atakukataa (Hosea 4:6). Hatari kubwa sasa iko mbele yetu sote, tunapaswa kutumia uhuru tuliopewa na Mungu kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya wokovu wetu.
Mungu akubariki unapoendelea kutafakari.
Next
« Prev Post
« Prev Post
First
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
EmoticonEmoticon